Mtoto Saimon Waziri mwenye umri wa miaka minne amefariki dunia na watu zaidi ya hamsini wamepata madhara kwa kula kitu kinachosadikika kuwa ni sumu ya Cyanaide inayotumika kuchenjulia dhahabu katika kijiji cha Busanda wilayani Geita.

Kwa kawaida sumu hiyo husafirishwa kwa taratibu za kiusalama na uangalizi mkubwa lakini kuna baadhi ya watu husafirisha kwa njia isiyo halali kama ilivyotokea katika tukio hilo ambapo ilisafirishwa kwa njia ya pikipiki ikiwa kwenye gunia dogo.

Hadi sasa kemikali hiyo imeshasababisha madhara hata kwa mifugo ambapo Kuku zaidi ya 60 na Mbuzi zaidi ya tano wamekufa.

Pasi kujua madhara wananchi wanaokota sumu hiyo kwa mikono na kuitupa shambani ili kuokoa mifugo yao.

Inadaiwa kuwa kemikali hiyo ilikuwa inatolewa Geita na kupelekwa katika kampuni ya Kisesa Gold Mine inayojishughulisha na uchenjuaji wa dhahabu iliyopo katika kijiji cha Rwamgasa, ambapo meneja wa kampuni hiyo Robert Marko alikana kwa kampuni hiyo kuhusika.

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita ACP Mponjoli Mwabulambo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na tayari watu wawili wanashikiliwa kwa uchunguzi zaidi.

Kaimu mkuu wa mkoa ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Geita Henry Kapufi ameagiza uchunguzi wa kina ufanyike na hapa anaagiza kukamatwa mmiliki wa kampuni hiyo pamoja na meneja.

Chanzo: ITV

Post a Comment

 
Top