Mambo yanaonekana kumwendea vizuri straika wa kimataifa anayekipiga katika timu ya KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, baada ya mashabiki kuzidi ‘kuishobokea’ jezi yake.

Tangu atue nchini Ubelgiji kukipiga katika klabu ya KRC Genk, nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania, amekuwa akitupia mabao kuisaidia timu yake kila kukicha, kiasi cha kuwavutia mashabiki ‘wazungu’ wa timu hiyo.

Mwishoni mwa wiki, nyota huyo alitokea benchi wakati timu yake ya KRC Genk ikiibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Kortrijk, kwenye mchezo wa Kundi B kuwania tiketi ya kucheza michuano ya UEFA Europa League mwakani.

Mashabiki waliomshuhudia nyota huyo walionyesha mabango uwanjani kumshabikia Samatta, huku moja likiwa limeandikwa maneno ya Kiingereza yaliyosomeka: “Please Samatta can I have your shirt Please,’ maneno yenye maana: “Samahani Samatta naweza kupata jezi yako tafadhali?”

Katika mechi hiyo Samatta aliingia dakika ya 66 kwenda kuchukua nafasi ya mfungaji wa bao la kwanza la Genk, kinda Mbelgiji, LeandroTrossard aliyefunga kwa penalti dakika ya 14 katika mchezo huo ambao mabao mengine mawili yalifungwa na kinda mwingine Mbelgiji, Siebe Schrijvers, dakika ya 45 na 70.

Samatta alianzia benchi baada ya mchezo uliopita kuanzishwa Jumatano, lakini hakufunga KRC Genk wakilazimishwa sare ya 1-1 na wenyeji, AS Eupen katika Uwanja wa Kehrweg mjini.

Genk inaendelea kuongoza Kundi B katika mchuano wa kuwania tiketi ya Europa League kwa pointi zake 16 sasa, baada ya kucheza mechi sita na Samatta jana ameichezea Genk mechi ya 55 tangu ajiunge nayo Januari mwaka jana kutoka TP Mazembe ya DRC akiwa amefunga mabao 18.

Kati ya mechi hizo 55, michezo 18 Samatta alicheza msimu uliopita na 37 msimu huu na kati ya hiyo, ni michezo 33 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na 23 msimu huu.

Mechi 21 kati ya hizo alitokea benchi, nane msimu uliopita na 13 msimu huu, wakati 11 hakumaliza baada ya kutolewa, tano msimu uliopita na sita msimu huu na katika mabao hayo 18, 12 amefunga msimu huu na sita msimu uliopita.
HALLA MBWANA SAMATTA

           Dimba

Post a Comment

 
Top