WAKATI Jumamosi ijayo Tanzania itasimama kwa muda wa dakika 90 ili kuwapa fursa mashabiki na wapenzi wa soka kufuatilia mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya Simba na Yanga, baadhi ya wachezaji wa zamani wa timu hizo wameibuka na kuuchambua.
Kwa nyakati tofauti, maveterani hao wameeleza mambo mbalimbali ambayo yanaweza kuufanya mchezo huo ukawa wa tofauti na wenye kujenga historia bora kwenye soka la Tanzania, kwani moja ya sifa za ‘derby ya Kariakoo’ ni kuweka historia ambayo haifutiki.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Sekilojo Chambua, anasema kwamba mchezo wa Simba na Yanga huwa ni mgumu, lakini unaweza ukawa mwepesi kama wachezaji wenyewe wakiamua kufanya hivyo.
“Mchezo wa Simba na Yanga huwa ni mwepesi kama mchezaji mwenyewe ukiamua kufanya hivyo, kwa mfano mimi nilikuwa nazipenda mechi hizo kutokana na urahisi wake, ndiyo maana nilikuwa naifunga sana Simba wakati wangu.
“Mchezaji mwenyewe unatakiwa kujiandaa kiakili na kutambua kuwa ni mechi muhimu, mimi nilikuwa nafanya hivyo na ilinisaidia kuifanya mechi hii kuwa nyepesi kwangu tofauti na mashabiki na watu wengine wanavyoiona.
“Yanga wanatakiwa kuwa makini na watulivu zaidi, hasa kwa mchezaji mmoja mmoja,” anasema Chambua, huku akiwataka makocha kuandaa vikosi vyao katika viwango vinavyotakiwa ili kupata matokeo bora.
Katika hatua nyingine, beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ yeye anaamini ni mchezo mgumu ambao unahitaji umakini wa hali ya juu, ingawa pia hauwezi kutabirika kirahisi kutokana na ukubwa wa mechi hiyo.
“Pamoja na mambo yote hayo, lakini ubora wa Simba hivi sasa unanishawishi kuamini kwamba, wanaweza kupata matokeo mazuri kufuatia uwezo ambao ameendelea kuuonyesha mshambuliaji Laudit Mavugo, ambaye siku hadi siku ameendelea kufanya vizuri katika mechi mbalimbali.
“Kitu pekee ambacho Yanga wanaweza kukifanya ni kuhakikisha kwamba wanaendelea kuimarisha safu yao ya ulinzi ili kuzuia makali ya washambuli wa Simba, ingawa washambuliaji wa Yanga wapo vizuri zaidi huku wakiwa na wastani mzuri wa kufunga kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara,” anasema Malima.
Naye Kipa wa zamani wa Simba, Moses Mkandawile, anasema kwamba ili timu zote ziweze kupata matokeo bora zaidi, ni vyema kuwa na maandalizi bora kuelekea kwenye mchezo huu.
Anasema kwamba si mchezo mwepesi, bali ukweli unahitaji maandalizi na umakini wa kweli, kwani kosa dogo linaweza kuigharimu timu moja na kuipa faida nyingine.
“Mchezo huu unahitaji maandalizi bora, ikiwamo utimamu wa mwili na akili. Lakini ninachokifahamu mimi ili kuweza kupata matokeo mazuri lazima pia wachezaji nao waweze kujituma na kujua nini wanachokwenda kukifanya uwanjani.
“Wito wangu kwa wachezaji wote wa Simba na Yanga ni kuuchukulia mchezo huu kwa umakini, lakini pia kwa timu zote mbili wapo wachezaji wa kuchungwa zaidi, kwani ndio wanaoweza kuwa sababu ya timu zao kupoteza mechi hiyo au kushinda kama wakiwabana vyema.
“Kwa upande wa Simba, wanatakiwa kumwekea ulinzi wa ziada winga wa kulia wa Yanga, Simon Msuva, ambaye kwa sehemu kubwa amekuwa ni sababu ya timu yake kupata ushindi, hivyo kama wakiweza kumdhibiti lango lao litakuwa salama.
“Vile vile Yanga inatakiwa kuwa makini na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, hasa kutokana na krosi zake ambazo mara nyingi zimekuwa zikileta madhara kwa timu pinzani,” anasisitiza nyota huyo wa zamani.
Nyota mwingine wa zamani wa Simba ambaye aliuzungumzia mchezo huo ni Fikiri Magoso, ambaye amesisitiza kwamba, ni mchezo usiotabirika, ingawa alikiri kuwa kikosi cha Yanga ni kizuri zaidi, ingawa Simba nao wanaendelea kuimarika na kufanya vizuri siku hadi siku.
“Ni mechi ngumu ambayo huwezi kuitabiri, lakini ina mambo yenye shinikizo kwenye maeneo matatu ambayo kwa sehemu kubwa yamechangia kuwepo kwa ugumu. Watu wenye shinikizo kwa sasa ni pamoja na wachezaji ambao wanataka kupata ushindi ili kuwapa furaha mashabiki wao.
“Lakini viongozi ambao kwa sehemu kubwa hivi sasa wanalazimika kuwa na timu zaidi ya wakati mwingine hata wale ambao hawakuwa wakionekana hivi sasa watakuwa anaonekana pamoja na mashabiki wanaohitaji kupata ushindi kwa timu yao,” asema Magoso.
Mchezo wa Jumamosi ni muhimu kwa sababu utaweza kuonyesha dira ya nani anaweza kutwaa ubingwa msimu huu katika Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao unashikiliwa na Yanga, iliyoutwaa mara 26, huku Simba ikitwaa mara 18 kwenye historia ya soka la Tanzania Bara.
Bingwa
Post a Comment