YANGA imeelezwa kuweka kambi kisiwani Pemba, kujiandaa na pambano lake na mahasimu wao wa jadi, Simba, huku kukiwa na taarifa za klabu hiyo kufanikiwa kufyatua mitego yote iliyowekwa na mahasimu wao.
Taarifa ambazo BINGWA limezipata kutoka ndani ya kambi hiyo, zinaeleza kuwa mara baada ya kutangazwa kwamba Yanga wanaweka kambi Pemba, mahasimu wao waliwatuma watu maalumu kwa ajili ya kuifuatilia Yanga kisiwani Pemba.
“Ni kweli awali tulisema kambi yetu itakuwa Pemba, lakini tuligundua kwamba mahasimu wetu Simba wametuma watu kwa ajili ya kufuatilia kila kitu tunachokifanya, kwa hiyo tumebadili utaratibu,” alisema mtoa habari wetu ambaye yupo na kikosi cha Yanga.
Alisema uongozi wa Yanga ulizipata taarifa za kuwepo mashushushu wa Simba kisiwani Pemba, ambao walitangulia mapema Alhamisi na hivyo wakaamua kuweka mkakati mzuri kuhakikisha vijumbe wao wa Simba wanaondoka kapa.
“Siwezi kusema mambo mengine, lakini kimsingi kambi yetu haitakuwa na mawasiliano yoyote na huu ndiyo mkakati, mambo mengine muulize Katibu Mkuu atakuwa na majibu,” alisema kiongozi huyo.
Mahasimu hao wa jadi kwenye soka la Tanzania watakutana Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, unaosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa soka wa maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, alisema wanalipa uzito mkubwa pambano hilo na kusisitiza kuwa kambi ya timu hiyo kujiandaa na pambano hilo itakuwa siri.
Alisema wameamua kufanya siri sehemu watakayoweka kambi ili kuepuka kufanyiwa hujuma na wapinzani wao.
“Hii imeshakuwa vita siwezi kukwambia kambi itakuwa sehemu gani, katika mazingira ya mechi kama hii hatuwezi kuruhusu mambo yafanyike hadharani kwa kuwa wapinzani wetu wanatafuta mbinu zetu,” alisema Mkwasa.
Mkwasa alisema wameamua kufanya hivyo ili kuepuka kuanika hadharani mambo yao na akisisitiza kuwa hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kuingia kambi ya timu hiyo zaidi ya wachezaji na benchi la ufundi.
“Kuna vitu tumeshaviona haviko sawa, hivyo katika kipindi hiki cha mapambano tunataka kufanya mambo yetu kwa usiri mkubwa pasipo adui zetu kujua nia na madhumuni kupata ushindi,” alisisitiza Mkwasa.
Kwa upande mwingine, mmoja wa matajiri wa timu hiyo ambaye pia hakupenda kutajwa jina lake gazetini, alisema Simba wamekuwa na presha kubwa sana na mechi hiyo ndiyo maana wamekuwa wakitafuta kila mbinu kuhakikisha wanaiua Yanga lakini hawatafanikiwa.
“Tumeshtukia mchezo wao wa kutuma watu Pemba na mitego yao tangu Alhamis iliyopita tumeitegua, sasa tunafanya mambo kimya kimya na kwa kifupi ‘tumekata’ mawasiliano kambini kwa hiyo hawatapata kitu,” anasema tajiri huyo.
Kigogo huyo alisema tayari wamejipanga kuwapa mamilioni ya fedha wachezaji wa Yanga, bila kutaja kiasi hicho cha fedha endapo wataibuka na ushindi siku hiyo.
“Tumeahidi kuwafurahisha wachezaji, si vyema kukitaja kiasi cha fedha tutakachowapa, tunahofia wasije wakaanza kupanga matumizi kabla ya mchezo lakini ni fedha nyingi sana tutawapa kushinda miaka yote, wafanye kazi yetu,” aliongeza kigogo huyo.
Alisisitiza kuwa hivi sasa wanasubiri kukutana na mwenyekiti wa timu hiyo ili kuangalia ni namna gani watakavyoweza kuwaongezea fedha nyingine mbali na zile za kwao walizonazo na kuahidi kuwapa wachezaji.
“Unajua sisi hatuna muda wa kuchangishana kupitia kundi ya WhatsApp, Yanga timu ya matajiri wanatokea matajiri kumi na kuweka mzigo mezani na mwenyekiti anaongezea, kazi inabaki kwa wachezaji kufanya kweli kushinda ili wapate mzigo huo,” aliseMa
Post a Comment