WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ameelekeza kuvuliwa nyadhifa viongozi wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kuanzia juzi(Julia 5, 2017) ili kutoa nafasi ya kusuka upya uongozi wa chombo hicho kikuu cha usimamizi wa michezo mbalimbali nchini.
Kutokana na uamuzi huo, Majaliwa ameagiza shughuli za BMT kwa sasa ziendelee kutekelezwa na sekretariati yake hadi hapo uongozi mpya utakapopatikana.
Kwa sasa sekretariati ya BMT inaongozwa na Mohammed Kiganja ambaye naye aliipata nafasi hiyo baada ya kutumbuliwa kwa Katibu Mtendaji aliyemtangulia Henry Lihaya, ‘aliyetumbuliwa’ na aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye. Lihaya ‘alitumbuliwa’ kwa kuhamishiwa wizarani.
Waziri Mkuu Majaliwa alitoa agizo hilo mjini Dodoma wakati wa hotuba yake ya kuahirisha shughuli za mkutano wa saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mkutano ambao pamoja na mambo mengine, ulijadili na kupitisha bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
“Leo hii naelekeza Baraza la Michezo Tanzania livunjwe (uongozi) na shughuli zake zitafanywa na sekretariati hadi hapo baraza jipya litakapoundwa,” alisema Waziri Mkuu.
Kwa kauli hiyo ya Waziri Mkuu, maana yake ni kwamba Mwenyekiti wa BMT, Dionis Malinzi, ambaye ni ndugu na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, moja kwa moja anakuwa ameenguliwa katika wadhifa wake huo. Jamal Malinzi na wenzake kadhaa kwa sasa wameshitakiwa kwa makosa kadhaa ikiwamo la kudaiwa kutakatisha fedha, makosa yanayohusishwa na uongozi wao katika soka.
Kazi za BMT ni zipi?
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lililoundwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Sheria Namba 12 ya Mwaka 1967 limepewa jukumu kubwa moja la kuendeleza michezo lakini katika mchanganuo maalumu.
Mchanganuo wa jukumu hilo ni kuendeleza, kustawisha na kudhibiti aina zote za michezo ya ridhaa kitaifa kwa ushirikiano na vyama au vikundi vya michezo vya ridhaa.
BMT itatekeleza jukumu hilo kwanza kwa kuhimiza na kutoa fursa za ushirikiano miongoni mwa vyama mbalimbali vya taifa; pili, kuidhinisha mashindano ya kitaifa na ya kimataifa katika michezo na matamasha yaliyoandaliwa na vyama vya kitaifa na vyama vingine.
Tatu; kuandaa, baada ya kushauriana na vyama vya kitaifa vinavyohusika, mashindano na matamasha ya kitaifa na kimataifa kwa nia ya kubadilishana uzoefu na kukuza uhusiano wa kirafiki na mataifa mengine na nne, ni kuamsha ari ya kupenda aina zote za michezo kwa ngazi zote.
BMT na uchaguzi wa sasa TFF
Katika mchakato wa sasa wa uchaguzi wa uongozi wa Chama cha Soka Tanzania, BMT imekuwa ikishiriki kwa mujibu wa majukumu yake kisheria na mara ya mwisho kutoa tamko kuhusu uchaguzi huo ilikuwa Juni 21, mwaka huu.
Katika tamko hilo lililotolewa na Katibu Mtendaji wa BMT, Mohammed Kiganja, baraza hilo liliunga mkono uchaguzi huo.
Hata hivyo, pamoja na kuunga mkono, BMT waliagiza TFF kuwaelekeza wagombea wake wote kuzipitia sheria za baraza hilo, kanuni za baraza na kanuni za usajili, hususani kanuni ya 8 (1) na (2).
Kanuni hiyo ya 8 (1) na (2), inaagiza kuwa endapo wagombea wote watakaoshinda nafasi wanazowania kwa sasa ndani ya TFF, hawana budi kuachia nafasi mojawapo katika uongozi wa mpira wa miguu katika ngazi ya wilaya au mkoa aliyoshinda awali.
“Uchaguzi huu usivuruge amani iliyopo nchini. Wagombea wakumbuke kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi,” ilieleza taarifa hiyo ya BMT iliyotolewa na Kiganja
Kwa mujibu wa taratibu, mara baada ya uchaguzi wa TFF kukamilika, viongozi walioshinda wanatakiwa kula kiapo cha utii, na kujaza fomu Namba 5 ya BMT ya utekelezaji majukumu yao kwa mujibu wa kanuni namba 8 (4) ya baraza hilo.
Post a Comment