Mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi anatarajiwa kuwasili Dar es Salaam usiku wa leo kwa ajili ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea klabu ya Simba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe ameSema, Okwi atatua nchini majira ya saa 3 usiku na moja kwa moja atakwenda kupumzika kabla ya Jumapili kukutana na viongozi wa Juu akiwemo Rais Evans Aveva.
“Mambo yote yanakwenda sawa na Okwi anatarajia kuondoka Uganda saa 12 jioni na atawasili saa 3, usiku na taratibu nyingine zitafuata,” amesema Hans Poppe.
Kiongozi huyo amesema mshambuliaji huyo anakuja wakati mazungumzo baina ya usajili wake yameshakamilika na kilichobaki ni kusaini kwa ajili ya kuichezea timu yao msimu ujao.
Amesema kumpata mchezaji huyo kutakiimarisha kikosi chao ambacho kwa muda mrefu kina kiu ya kuona wanatwaa ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.
Amesema kwa usajili waliofanya msimu ujao wanataka kuwa moto wa kuotea mbali na kutawala soka la Tanzania kama ilivyokuwa kwa wapinzania wao Yanga ambao wanaonekana kupoteana kutokana na kujiondoa kwa mfadhili wao Yusufu Manji.
Hiyo itakuwa ni mara ya Tatu kwa Okwi kurudi Simba kwani awali aliondoka na kujiunga na Etoile du Saheal lakini baadaye aliachana na timu hiyo na kujiunga na Yanga ambapo alidumu kwa muda mchache kabla ya kurudi Simba alipodumu kwa msimu mmoja na kutimkia Denmark na baada ya kushindwa kufanya vizuri anarudi tena msimbazi.
source;goal
Post a Comment