HEKA heka za usajili zinaonekana kupamba moto kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, huku hadi sasa Simba wakitajwa kufanya kufuru kwenye suala hili.

Simba inaonekana kutisha baada ya hadi sasa kuwanasa wanandinga Jamal Mwambeleko na Emmanuel Mseja  wanaotoka Mbao FC, Yusuph Mlipili wa Toto Africans, John Bocco, Shomary Kapombe na Aishi Manula (hajatangazwa) wakitokea Azam FC  pamoja na Ally Shomary aliyekuwa akikipiga Mtibwa Sugar.

Mbali na wanandinga hao, tayari zipo taarifa za ujio wa aliyewahi kuwa straika wao, Mganda Emannuel Okwi, Donald Ngoma aliyemaliza mkataba Yanga na Haruna Niyonzima ambaye anatajwa kuingia mkataba wa miaka miwili na Wanamsimbazi hao.

Ni jambo lililo wazi hivi sasa kila shabiki, mwanachama na hata viongozi wa Simba wamejawa na furaha kutokana na jinsi wanavyokijenga kikosi chao kwa kusajili wachezaji ambao timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara inatamani kuwa nao.

Ujio wa Okwi, Ngoma na Niyonzima unaonekana kuleta matumaini makubwa zaidi ndani ya timu hiyo katika kutimiza lengo la kumaliza ukame wa mataji ulioonekana kuwaandama kwa misimu minne mfululizo.

Ni ukweli usiofichika katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Simba imepitia vipindi vigumu hali iliyosababisha kukosa hata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho barani Afrika yanayowakilishwa na mshindi wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa hapa nyumbani kabla ya kubadilishwa mfumo huo mwaka jana na bingwa wa Kombe la Shirikisho linaloandaliwa na TFF, maarufu FA kupewa nafasi.

Wakati kukiwa na taarifa Okwi na Ngoma watatua nchini leo kwa ajili ya kujiunga na Simba huku Niyonzima akitajwa kuwa tayari ameshaanguka saini ya miaka miwili Msimbazi, swali la kujiuza ni je, wanandinga hao wataweza kumaliza ukame wa mataji Simba?

Unaweza usiliwaze hili kwa haraka lakini ni kitu muhimu kwa faida ya klabu hiyo iliyoonekana kuwa na uchu wa kutwaa Kombe la Ligi Kuu Bara pamoja na lile la Shirikisho.

Siku zote inafahamika ili mchezaji aweze kufanya kazi yake kiufanisi, lazima apate ushirikiano kutoka kwenye benchi la ufundi, uongozi na wachezaji wenzake lakini pia aweze kutimiziwa mahitaji yake muhimu jambo linaloonekana ni tatizo kubwa kwenye klabu zetu kongwe za Simba na Yanga.

Si mara moja tumesikia wanandinga wa timu hizo wakigoma kucheza kutokana na masuala hayo ambayo ni magonjwa sugu kwa hivi sasa.

Ni wazi kama Niyonzima, Okwi na Ngoma watakuwa wamejiunga Simba bila ridhaa ya benchi la ufundi hawawezi kufanya kazi zao kiufanisi, kwani huenda kocha asiwatumie vile inavyotarajiwa.

Masuala kama kutolipwa haki zao kwa wakati linaweza pia kuwaathiri kwa kuwa inafahamika wazi wamekuja Tanzania kutengeneza fedha na si kufurahisha mashabiki.

Kubwa kuliko yote ni suala la tabia za viongozi kuingilia majukumu ya benchi la ufundi ambayo si mara moja  wamekuwa wakilalamikiwa, lakini pia jambo hili limekuwa likitengeneza chuki baina ya benchi la ufundi, wachezaji na mabosi wa timu.

Iwapo kama Simba watawasajili wanandinga hao kisha kufanya vitu vinavyoweza kuharibu utendaji wao wa kazi kufanyika Okwi, Ngoma na Niyozima hawataweza kumaliza ukame wa mataji Simba hata kama watapata ushirikiano kutoka kwa wanandinga wenzao.

Post a Comment

 
Top