MANCHESTER, England
Ndio, kwanza tukiri United ilistahili bao la kusawazisha la Zlatan Ibrahimovic pale Old Trafford dhidi ya Everton.
Sawa, wanafanya kila wawezalo ili kuilinda rekodi ya kutopoteza mchezo hadi sasa.
Lakini mbona inazidi kuonekana ni kitu cha kawaida? Kwanini hakuna furaha ya kweli Old Trafford? Maswali yanayostahili majibu yenye haki.
Kwa kipindi ambacho Jose Mourinho, amekaa pale United, tumekuwa mashuhuda wa jinsi anavyohangaika na mifumo ili kutafuta suluhisho la changamoto inayomgandisha sehemu moja kwa msimu wote huu.
Changamoto yenyewe ni kuisuka United yenye makali kwenye ushambulizi na kuiwezesha iwe timu imara.
Kwa sehemu aliyopo, uzoefu wake na kipaji chake cha ufundishaji, Mourinho asingeshangaza kama angeweza kuifanya United ikawa imara zaidi ya ilivyo sasa. United ilitakiwa kuwa timu tishio zaidi. Hilo halikutegemewa kuwa jukumu zito sana kwa Mourinho hadi sasa.
Lakini kitu kinachoendelea kuumiza mioyo ya mashabiki wa United ni jinsi wanavyoiona timu yao ikihangaika kusawazisha bao dakika za mwisho dhidi ya Everton.
Huu ndio msimu wake wa kwanza, kila mchezo wanaocheza lazima kuwe na hali ya woga wa kufanya kweli. Utetemeshi unaowagharimu siku baada ya siku.
Woga wa kufanya kweli ndio huo unaowazalishia mabao ya penalti za dakika za lala salama. Sawa, sare tisa na mabao 21 ndani ya mechi 16 za ligi ni rekodi nzuri ya kujisifu, lakini itawasaidiaje United kumaliza ndani ya ‘top four’.
Jibu ni rahisi: Hawataweza.
Hata kama lilikuwa ni jukumu la Ibrahimovic kufunga ile penalti, bado United ina utegemezi mkubwa kwake. Asipokuwa kwenye fomu nzuri, United kupata ushindi ni ndoto.
Asipokuwepo Jesse Lingard, Anthony Martial na Marcus Rashford, wanashindwa kabisa kufanya la maana! Wanachefua.
Hebu tazama hii: Kwa jinsi ambavyo Romelu Lukaku na Ross Barkley walivyokuwa wakijaribu kuisumbua ngome ya United, ingekuwaje kama wangepata bao.
Hakika walikuwa bora zaidi usiku wa Jumanne kuliko hata walivyocheza na Liverpool.
Kwa umoja wao walipambana kuisumbua sana ngome ya United hadi walipopata bao kupitia kwa Phil Jagielka.
Hapo wakaipa mtihani United. Waanzie wapi kulisawazisha bao. Waanzie wapi kuwafurahisha mashabiki waliojazana Old Trafford.
Lilikuwa ni bao la kizembe. Marouane Fellaini alimruhusu vipi Williams kujaribu kuucheza ule mpira wa kona? Marcos Rojo, alikubali vipi kumkaba kiulaini vile Jagielka? Ukabaji wa aibu.
Kama Lukaku na Barkley wangekuwa ‘smart’ katika mashambulizi yao, kama wangekuwa na maamuzi ya ‘kiutu uzima’ pindi walipofanya mashambulizi ya kushtukiza, ushindi ungewaendea wao.
Lakini kutokana na ugumu wa mchezo wenyewe, walishindwa kufanya hivyo. Ni nani alisubiriwa kufanya chochote kitu United igeuze matokeo? Ni Mourinho.
Kumbe tayari alishapagawa, asielewe la kufanya. Mabadiliko ya kumwingiza Paul Pogba yalikaribia kusababisha mengine lakini nani wa kumsaidia Pogba. Mourinho hapo hakujua ampe nani jukumu hilo.
Ghafla akamwinua Luke Shaw! Yalikuwa ni mabadiliko yaliyochagizwa na maamuzi ya kuchanganyikiwa. Maamuzi ya kawaida sana.
Labda haikujulikana kama Shaw angekuja kusababisha penalti kwa shuti alilopiga na kuguswa na mkono wa Williams. Yote kwa yote lilikuwa ni jukumu la Zlatan kurudisha uhai wa United.
Mourinho aliposubiriwa kuzungumza kitu kipya juu ya mwenendo wa United na nini kitakachofanyika, akasikika akikumbushia mashuti yaliyogonga mwamba, eti mabao yaliyokataliwa kisa ‘offside’, mara akatukumbushia kiwango safi cha kipa wa upinzani.
Eti alishangazwa na mfumo wa kujilinda wa Everton. Yote hayo ni blah, blah, blah.
Bora angenyamaza tu. Kilichotarajiwa OT ni tofauti na kinachoonekana.
United imekuwa ya kawaida tu.
source;bingwa
Post a Comment