UKISIKIA pesa inaongea katika pambano la soka la watani wa jadi hapa nchini, Simba na Yanga, ujue ni kweli. Hali hii inatokana na timu hizo kutumia mamilioni ya fedha kusaka ushindi ndani na nje ya uwanja kwenye mechi baina yao.
Pamoja na kwamba pambano baina ya miamba hiyo ni keshokutwa, limetawaliwa na fedha kutoka kila upande, Simba wameweka kambi Zanzibar na Yanga wako Kigamboni jijini Dar es Salaam, lakini kila timu inahaha kweli kweli kukusanya na kutawanya fedha za mipango ya kujihakikishia ushindi.
Uchunguzi wa BINGWA umebaini kwamba jijini Dar es Salaam, Simba na Yanga zinachangishana fedha kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo makundi ya WhatsApp, matawi, matajiri na hata viongozi.
Simba ambayo imeweka kambi Zanzibar pamoja na timu yao kufanya maandalizi visiwani humo ambako inapata sapoti ya wanachama wa huko, lakini nguvu kubwa inatokea kwenye matawi ya Dar es Salaam ambayo yamekuwa yakichangishana fedha na kufanya vikao vya usiku na mchana kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo huo.
BINGWA limenasa dondoo kwamba kwenye matawi kila mwanachama amehimizwa kuchangia japo Sh 5,000 na tayari mpango huo unakwenda vizuri ambapo baadhi ya fedha za awali zilizopatikana zimepelekwa panapohitajika kuongeza nguvu ya maandalizi wakati nyingine zikiendelea kukusanywa.
Inaelezwa kwamba, lengo la Simba kukusanya fedha nyingi ni kuhakikisha wanajiweka sawa katika kila eneo ambalo linahitaji fedha, ikiwemo kuwapa motisha wachezaji wao, kununua kila bao litakalofungwa pamoja na mambo mengine.
Wakati Simba wakiwa kwenye mkakati huo kwa upande wa Yanga wao wamechangishana fedha kwenye matawi, huku kila tawi likitakiwa kupanga mipango yake ya kupatikana ushindi na kwamba uongozi wa Yanga makao makuu umeongeza nguvu kwenye mfumo wa matawi ili kuhakikisha ushindi unapatikana.
Maandalizi ya mechi hii yamekuwa ya aina yake kwa timu zote mbili, ambapo ushirikishwaji umekuwa mkubwa kwa matawi na wanachama kwa kila timu huku wakiamini kwamba kila sehemu ina umuhimu wake.
Pambano hili la keshokutwa limekuwa na maandalizi yenye gharama kubwa sana kwa wakati huu kutokana na ukweli kwamba ndilo linaloelezwa kutoa mwelekeo wa ubingwa kwa msimu huu, hivyo kila timu imeweka nguvu ya kutosha kwenye maandalizi yake ya ndani na nje ya uwanja.
Ingawa timu zote zimekuwa zikitawanya fedha, lakini bado maandalizi yamekuwa hayafafanuliwi kwenye mawasiliano ya kwenye makundi ya wanachama wa timu hizo jambo ambalo linaonyesha wazi kwamba si maandalizi ya uwanjani pekee yanayofanyika.
Katika mtanange wa awali timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 katika mzunguko wa kwanza kwa mabao yaliyofungwa na Amissi Tambwe dakika ya 23 kabla ya Shiza Kichuya kuwasawazishia Wekundu wa Msimbazi dakika ya 87.
Wakati makocha wa timu hizo wakiwa na kazi ya kuhakikisha wanavinoa vikosi vyao vilivyo ili waweze kupata pointi tatu muhimu, mabosi, wanachama na vigogo kutoka ndani ya Serikali wanadaiwa kufanya mipango yao nje ya kambi.
BINGWA lilipotaka kujua fedha hizo nyingi zinakusanywa kwa ajili ya nini hasa? Ilikuwa ngumu kupata ukweli ingawa baadhi ya wadau wake walilipasha kwamba kwa Simba wananunua kila bao litakalofungwa na pia wamejipanga kununua ushindi mzima kama utapatikana.
“Kwa kawaida Simba tuna kawaida ya kutoa motisha kwa wachezaji wetu kila wanaposhinda mchezo na hili lipo wazi lakini hivi sasa licha ya kuwapa wanandinga kiasi cha fedha kitakachopatikana baada ya kushinda, tumeamua kufanya maandalizi mengine na tutanunua kila bao litakalofungwa maana tunajua umuhimu wa mechi hii kuelekea katika ubingwa,” alisema mtoa habari wetu.
Naye mmoja wa wajumbe wa kamati ya mashindano wa Yanga ambaye hakutaka kutajwa jina, ameliambia BINGWA kuwa: “Wapo wanachama, mashabiki, viongozi waliopo serikalini na uongozi wa juu wa timu kwa pamoja tumeamua kuiwezesha timu kifedha ili iweze kupata ushindi katika mchezo wa Jumamosi.”
Alisema wao hawana mpango wa kununua mabao yatakayofungwa, lakini wanainunua mechi yote kwa kuwa wanajua kilichopo mbele yao na ndiyo maana wameshainunua mechi yote kwa kuwaahidi wachezaji wao kiasi kinono cha fedha.
Kwa upande wa waamuzi, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nalo limeahidi kutoa donge nono kwa waamuzi watakaochezesha mchezo huo, wakichezesha mchezo vizuri kwa kufuata sheria 17, huku likiwafanya kuwa siri kubwa kuogopa waamuzi hao kusumbuliwa na vigogo wa timu hizo.
Bingwa
Post a Comment