KATIKA mambo yanayozungumzwa zaidi kila linapokaribia pambano la timu kongwe nchini, Simba na Yanga, zenye utani wa jadi tangu zilipoasisiwa, Yanga 1935 na mwaka mmoja baadaye 1936 Simba ikazaliwa, ni kila upande kutangaza kumtandika mwingine.
Siku na saa za kufanyika kwa mpambano huo zinazidi kukimbia na pale itakapotimu siku ya Jumamosi Februri 25 majira ya saa 10 alasiri, hadithi hiyo itakuwa siyo ya kufikirika tena, kwani itasubiri dakika 90 tu kupata jawabu lililokuwa likiumiza vichwa vya mashabiki.
Tangu zilipoanza kukutana kwa mara ya kwanza mwaka 1965, ambapo Yanga iliweza kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0, dhana ya utani wa jadi ambao muda mwingine huwa na uhasama ndani yake ilianza kujitokeza kwa nguvu kubwa.
Kwa mashabiki wa Simba, pamoja na kuwa takwimu zinazonyesha Yanga ndiyo inayoongoza kupata ushindi mara nyingi zaidi ya Simba, lakini bado wana kumbukumbu nzuri ya kuiadhibu Yanga kwa idadi kubwa ya mabao.
Simba bado wanaiota rekodi inayochosha kutokana na kudumu kwa muda mrefu, ambapo Wekundu hao wa Msimbazi waliichapa Yanga kwa jumla ya mabao 6-0 na kusababisha mtafaruku mkubwa ndani ya klabu hiyo ya Jangwani.
Haya yalikuwa ni matunda ya mpasuko kwa klabu ya Yanga uliojitokeza mwaka 1976 na kupelekea kuanzishwa kwa timu ya Pan Afrika, iliyoondoka na wachezaji wengi muhimu na kuicha Yanga ikiwa na hali mbaya.
Wachezaji waliokuwa mastaa wa Yanga walikwenda Pan kwa kumfuata aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Tabu Mangara na kuiacha Yanga ikisajili upya wachezaji ambao hawakuwa na vigezo na hivyo kuambulia aibu hiyo kubwa ya kihistoria kutoka kwa Simba.
Rekodi Ya mabao sita, huku Kibadeni akipiga mabao 3 inaendelea kupoteza sifa kutokana na kudumu kwa muda mrefu, na pia inathibitisha udhaifu kwa washambuliaji waliowahi kupita katika kikosi cha Simba kwa vipindi tofauti, lakini wakashindwa kuifuta.
Ilikuwa ni Julai 19, mwaka 1977, kiasi cha miaka 35 iliyopita, wakati mshambuliaji hatari wa Simba, Abdalah Kibadeni, alipoifungia timu yake mabao 3 dhidi ya Yanga na kuufanya mchezo huo kumaliza kwa timu hiyo ya Msimbazi kushinda kwa jumla ya mabao 6-0.
Simba enzi hizo ilikuwa ikinolewa na kocha anayekumbukwa kwa mafanikio makubwa, Dimitar Samsarov.
Mabao ya Simba siku hiyo yaliwekwa kimiani na Abdallah Kibadeni katika dakika za 10, 42 na 89, Jumanne Hassan ‘Masimenti’ dakika za 60 na 73, na Selemani Sanga wa Yanga aliyejifunga mwenyewe dakika ya 20. Kipigo hicho kilikuwa kichungu zaidi kwa kipa wa Yanga, Benard Madale, ambaye alitupiwa virago baada ya mechi hiyo.
Rekodi yake haijavunjwa hadi hii leo, lakini Kibadeni mwenyewe anatamani kuona washambuliaji wapya wakiandika rekodi nyingine na kuifuta hiyo ya kwake.
Mara nyingi mchezaji huyo wa zamani ambaye kwasasa ni kocha mashuhuri nchini na amekuwa akifundisha klabu mbalimbali amekuwa akieleza kutoridhishwa na juhudi binafsi za washambuliaji wa sasa.
Kutokea zama za Kibadeni hadi hivi sasa Simba imewahi kupata mastraika wazuri ambao katika mechi kama hii ya watani wa jadi wameishia kupata mabao mawili, miongoni mwao ni
Mganda Emmanuel Okwi, aliyefunga mabao mawili yaliyonogesha ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Yanga, Mei 2012.
Rekodi ya Okwi inapewa heshima zaidi Msimbazi kutokana na kuwa ushindi mkubwa, lakini pia bao lake la kwanza alilifunga katika dakika ya kwanza sekunde ya 10 na pia mabao yote mengine yaliyoleta ushindi huo yalikuwa ni msaada wa Okwi.
Wapo mashabiki wa Simba, akiwamo aliyewahi kuwa mtunza hazina kwenye miaka ya 1980, Seiifudin Jamal, ambaye anaamini kwamba rekodi ya Kibadeni ipo karibu kuvunjwa.
Jamal ameanza kuitabiria kipigo Simba katika mchezo wa Februari 25, akisema utawaletea furaha ambayo hawajaipata kwa kipindi kirefu.
Dimba
Post a Comment