Leo katika matini, tunakuletea hadithi ya kupendeza sana ya mtu jagina  ulimwenguni, ajulikanaye katika ushupavu wa biashara kwa jina la Jack Ma. Kwa simulizi hii ya kupendeza, ongozana nami, msimulizi, Jerry Mshiu, kukupatia kile kilicho kizuri, ambacho bila shaka, kitayang’arisha macho yako.

 Image result for jack ma imagesImage result for jack ma imagesImage result for jack ma images

Jack Ma ni jina mashuhuri hasa China na pia ulimwenguni. Jack Ma ni jina la utani tu alilopewa na mbaruzi akiwa angali kijana mdogo. Jina lake asilia alilotunukiwa na wazazi wake wapendwa ni Ma Yun. Ma ni mfanyabiashara mahiri wa Kichina, aliyeasisi na sasa akiwa Mwenyekiti Mtendaji (CEO) wa Alibaba Group. Yamkini, Ma, ndiye mjasiriamali mbobevu wa kwanza wa Kichina kutolewa katika kurasa za Jarida la Kibiashara la Forbes la nchini Marekani.

Ma alizaliwa katika jimbo la Zhejiang lililopo Mashariki mwa China. Akiwa angali kijana mdogo, Ma, alijifunza kwa vitendo lugha ya Kiingereza, akizungumza kila siku na wazungumzaji wazawa wa lugha hiyo (Natural English Speakers) katika hoteli moja iliyokuwa karibu na masikani yao. Ili kujiimarisha na kukimudu Kiingereza barabara, Ma, alifanya kazi ya kuwatembeza wabaruzi hao bila malipo katika viunga vya jiji la Zhejiang. Alifanya hivyo kwa miaka kenda. Ni katika wasaa huo ambapo mmoja kati ya wabaruzi alimpachika jina hilo la Jack Ma, kwa kile kilichodaiwa kuwa jina lake lilikuwa gumu kidogo kulitamka, yaan mbaruzi huyo alishindwa kutamka, Ma Yun, badala yake kutamka Jack Ma ili kurahisisha.

Baadaye, angali akiwa kijana wa wastani, Ma alishindwa mara tatu mtihani wa kujiunga elimu ya juu, yaani Chuo Kikuu.

Ma alijiunga katika Taasisi ya Ualimu iliyoitwa Hangzhou Teacher’s Institute ambayo kwa sasa hujulikana kama Hangzhou Normal University.  Hatimaye, mwaka 1988, akahitimu Shahada ya Kwanza ya Sanaa katika Kiingereza (B.A in English).

Punde, baada ya kuhitimu, Ma alianza kufanya kazi ya ukufunzi wa lugha ya Kiingereza na biashara za kimatifa (International trade)  katika Chuo Kikuu cha Hangzhou Dianzi.  Hata hivyo baadaye akajiunga na skuli ya biashara (CKGSB) kilichopo Beijing-China na kuhitimu mnamo mwaka 2006.

Alipohitimu masomo yake, Ma alituma maombi ya kazi tofauti, thelathini, ilhali hakupata hata mojawapo. Pengine, Ma anamsimulia rafikiye Rose, kisa fulani kilichohusiana na masuala ya kazi: “Kuna wakati fulani nilikuwa na wanzangu wapatao ishirini na wanne, tulienda kuomba kazi sehemu fulani. Wote walibahatika kupata isipokuwa mimi pekee. Ilistaajabisha.”

Mnamo mwaka 1994, Ma alisikia habari kuhusiana na masuala ya intaneti. Ndiposasa, mwanzoni mwa mwaka 1995, Ma akasafiri kwenda Marekani na rafikize ambao walimsaidia kuingia mtandaoni. Kwa mara ya kwanza alipoingia katika intaneti, alitafuta neno ‘beer’. Ilhimu alipata maeelezo kuhusiana na neno hilo, alishangazwa kutopata maelezo ya nanma hiyo kutoka katika nchi yake, China. Ndipo alienda mbele zaidi, kutahuta habari za jumla zilizohusiana na China. Alistaajabishwa zaidi alipoona hakuna chochote kile.
Kwa mantiki hiyo sasa, Ma na rafikize wakaamua kuunda tovuti duni iliyohusiana na (mambo ya) China. Saa nne hivi baada ya kuunda tovuti hiyo, Ma alipokea barua pepe kadhaa kutoka kwa baadhi ya Wachina wakitaka kujua habari kuhusu yeye.

Mnamo Aprili 1995, Ma, mwenzi wake na rafikize walipata dola za Kimarekani 20,000/= na kuanzisha kampuni ya intaneti waliyoiita China Yellow Pages. Kampuni hii ililenga kuunda tovuti kwa minajili ya kampuni za Kichina. Ndani ya miaka mitatu, walijikusanyia jumla ya fedha za Kichina (Yuan), 500, 000/=, ambazo ni sawa na dola za Kimarekani 800,000/=

Mnamo mwaka 1998 hadi mwaka 1999, Ma aliteuliwa kuwa mkuu wa teknolojia ya habari katika kampuni iliyoanzishwa na China International Electronic Commerce Center kwenye kitengo cha Ministry of Foreign Trade and Economic Cooperation. Licha ya wadhifa aliopewa, mnamo mwaka huohuo, 1999, Ma aliacha wadhifa huo adhimu. Baada ya kujiengua, Ma, alirejea Hangzhou akiwa na jopo lake (rafikize) na kuanzisha kampuni ya Kibiashara ya Alibaba.  Vyanzo mbalimba vinaeleza kuwa Bw. Ma, alianzisha kampuni ya Alibaba kwa mtaji wa fedha za Kichina (Yuan), 500,000/= sawa na dola za Kimarekani 800,000/=

Mnamo Oktoba 1999 hadi Januari 2000, Alibaba ilishinda mara mbili jumla ya dola za Kimarekani 25 milioni katika programu iliyoanzishwa na International Venture Capital Investment. Programu hii ilianzishwa ili kusaidia kunyanyua biashara katika masoko ya ndani ya China, hasa ikilenga kunyanyua makampuni ya Kibiashara madogo na yale ya darajia la kati. Mnamo, 2003, Ma alianzisha kampuni nyingine ambazo ni Taobao, Alipay, Ali mama na Lynx, ambazo zote zinahodhiwa na kusimamiwa na Kampuni ya Alibaba. Tuseme, kampuni hizi ni kama matawi ya Kampuni ya Alibaba.

Na ilipofika mnamo mwaka 2014, iliripotiwa kuwa Alibaba ilikuza hisa zake na kufikia zaidi ya dola za Kimarekani 25 bilioni katika mauzo ya hisa ya New York (New York Stock Exchange).

Kwa sasa, Ma anahudumu kama mwenyekiti mtendaji (CEO) wa Alibaba Group, akikadiriwa kuwa na utajiri wa zaidi ya dola za Kimarekani 28 bilioni.  Hadi hivi sasa, Alibaba Group inahodhi matawi tisa ya kibiashara ambayo ni: Alibaba.com, Tmall, eTao, Alibaba Cloud Computing, Juhuasuan, 1688.com, Aliexpress.com na Alipay.

 Image result for jack ma imagesImage result for jack ma imagesImage result for jack ma images
Kabla ya kufikia tamati, ndugu msomaji mwema, katika ukuruba wa jitihada nyingi, Bw. Ma amepata mafanikio makubwa si utani, ambapo miongoni mwetu tungalijisikia msisimko na kujivunia iwapo tungaliyafikia kabla hatujatoweka katika dunia hii ya madhila lukuki. Mafanikio ni mengi. Vivyo basi, tutakuletea finyu tu:
~2004: Ma, alichaguliwa na Kituo cha Runinga cha China, (China Central Television), kuwa miongoni mwa wafanyibiashara kumi bora zaidi wa mwaka.
~2005: Ma, aliteuliwa na Jukwaa la Uchumi la Dunia (World Economic Forum) kuwa kiongozi wa vijana duniani. Pia, mwaka huo huo, Ma, alitajwa kuwa miongoni mwa wafanyibiashara 25 wenye nguvu zaidi katika Bara Asia.
~2008: Ma, alitajwa na shirika la Barron’s kuwa miongoni mwa wenyeviti watendaji 30 walio bora zaidi duniani ( 30 Best World’s CEO).
~2009: Ma, aliorotheshwa na The time, kuwa miongoni mwa watu mia moja (100) wenye ushawishi mkubwa zaidi kwa watu duniani.
~2010: Ma, aliteuliwa na Forbes Asia, kuwa miongoni mwa mashujaa wahisani katika majanga na umasikini.
~Ma, alizawadiwa shahada ya tatu ya heshima (Ph.D.) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Ulimbe cha Hong Kong ( Hong Kong University of Science and Technology).
~2015: Ma, alipewa tuzo yaMjasiriamali bora wa mwaka ijulikanayo kama The Asian Award.
~2016: Ma, aliteuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) kuwa mshauri kiongozi wa masuala mbalimbali yahusuyo vijana duniani, kazi ambayo anahudumu mpaka sasa.

Katika maisha binafsi (personal life), Bw. Ma alibahatika kumwoa Bi. Zhang Ying ambaye alikutana naye pindi alipokuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Hangzhou. Tuseme, walisoma chuo kimoja. Kwavyo, wamezawadiwa watoto wawili, mmoja binti na mwingine mwanamume.

Kwa mujibu wa yeye mwenyewe, Ma, anapendelea sana kucheza michezo ya kimapigano ya kichina, yaitwayo Tai Chi, ambayo alijifunza angali akisoma katika Chuo Kikuu cha Hangzhou. Inasemekana kwamba, Wang, Jet Li na mwenyewe Ma, huendesha mafunzo ya mchezo huo kwenye kampuni yake ya Alibaba, na kila mfanyikazi hulazimka kisheria kushiriki.

Kulingana na maelezo ya msaidizi wake, maono ya Ma ni kuwa mkufunzi mahiri wa Tai Chi, na angalipenda watu wamfahamu zaidi kwa mchezo huo kuliko anavyofahamika sasa kama mfanyibiashara bilionea.
Shukrani: pole sana kwa kuchosha nap engine kuchukua muda wako kwa kusoma makala hii ndefu kiasi, yenye wastani ya kurasa nne ama tatu hivi. Tunatumai kuwa utakuwa umependezwa kwa namna fukani. Na, ni furaha yetu utakuwa umejifunza mambo mawili ama matatu. Alamsiki.

 Image result for jack ma images




Post a Comment

 
Top