Kuondoa adhabu ya kifo nchini Burundi kuko mashakani - IWACU- Burundi
Wakati dunia ikiadhimisha siku ya kupambana na adhabu ya kifo, juhudi za kuendelea na marufuku ya adhabu hiyo nchini Burundi zimeingia doa, baada ya mauaji kiholela kuendelea kutokea, na sauti za kutaka adhabu hiyo iridushwe zikianza kusikika. Burundi ni moja ya nchi chache za Afrika zilizofuta adhabu ya kifo. Jumuiya ya kuhimiza haki za binadamu ya nchi za maziwa makuu imezipongeza Burundi na Rwanda kwa kuondoa adhabu ya hiyo, hata hivyo imelalamika kuhusu mauaji ya kiholela yanayotokea katika nchi hizo, yanayofanywa na makundi ya watu wanaomiliki silaha kiharamu na maofisa wa idara za usalama.
Bunge la Rwanda lawaomba wabunge wa Ulaya waondoa azimio la kuilaani Rwanda- The Times of Rwanda- Rwanda
Bunge la Rwanda limepitisha kwa kauli moja azimio kulitaka bunge la Umoja wa Ulaya kuondoa azimio la kuituhumu Rwanda kuwanyanyasa wanasiasa wa upinzani. Hatua hiyo imefikiwa baada ya bunge la Umoja wa Ulaya kupitisha azimio lenye kurasa tano linalosema serikali ya Rwanda inahusika na vitisho, kuwakamata, au kuwahukumu viongozi wa vyama vya upinzani, wanachama wao, wanaharakati, na hata waandishi wa habari wanaodhaniwa kuwa ni wapinzani wa serikali. Moja ya mifano iliyotolewa na azimio hilo la umoja wa Ulaya ni Bibi Victoria Ingabire anayetumikia kifungo cha miaka 15 kwa kosa la kukosoa msimamo wa serikali kuhusu mauaji ya halaiki ya mwaka 1994.
Uganda yaitaka Marekani itoe ripoti kuhusu mauaji ya raia wa Uganda aliyepigwa risasi- Daily Monitor- Uganda
Serikali ya Marekani imeahidi kuhimiza kutolewa kwa matokeo ya uchunguzi kuhusu mauaji ya raia wa Uganda Bw Alfred Orengo aliyeuawa kwa kupigwa risasi mwishoni mwa mwezi uliopita. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imekabidhi barua ya rambirambi. Orengo aliuawa na polisi baada ya mtu asiyejulikana kuwapigia simu polisi akisema kuna mtu anayehatarisha maisha yake na ya waendesha magari. Muda mfupi baada ya kufika polisi walifyatua risasi na kumuua. Lakini mashuhuda walisema Bw Orengo hakuwa na bastola.
Watu 10 wameuawa baada ya jeshi DRC kupambana na waasi wa ADF kutoka Uganda – New Vision- Uganda
Watu karibu 10 wameuawa kwenye mapambano kati ya jeshi la jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wapiganaji wa kundi la kiislamu la ADF kutoka Uganda. Waasi wa kundi la ADF walivamia mji wa Beni na kuwaua raia wanane, mwanajeshi mmoja wa jeshi la serikali aliuawa na muasi mmoja aliuawa. Mji wa Beni wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umekuwa ukitatizwa na matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu yanayofanywa na makundi mbalimbali, yanatumia fursa ya migogoro ya kikabila kuvuna raslimali za madini na misitu.
Mfumuko wa Bei nchini Tanzania kwa mwezi Desemba wafikia asilimia 4.5 - Habari Leo- Tanzania
Mfumuko wa bei nchini Tanzania kwa mwezi Septemba, umepungua hadi kufikia asilimia 4.5 kutoka asilimia 4.9 za mwezi Agosti mwaka huu. Hiyo inamaanisha kwamba kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2016 imepungua, ikilinganishwa na kasi ya mwaka ulioishia Agosti, mwaka huu. Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii, Bw Ephraim Kwesigabo alisema Dar es Salaam jana kuwa kupungua kwa mfumuko wa bei, kunahamasisha ukuaji wa uchumi. Kupungua huko kwa mfumuko wa bei kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia pamoja na sera ya serikali ya kuhakikisha fedha zinaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, badala ya kukaa kwenye mifuko wa watu binafsi.
Ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki, Kenya mfumuko wa bei umeongezeka kutoka asilimia 6.2 had 6.3, Uganda umepungua na kufikia asilimia 4.2, na Rwanda umepungua kutoka asilimia 6.8 hadi asilimia 5.8.
Walimu 18 wahojiwa kufuatia mikasa ya kupigwa wanafunzi Mbeya- Mwananchi- Tanzania .
Sakata la mwanafunzi wa shule moja ya kutwa mkoani Mbeya kupigwa na walimu limechukua sura mpya baada ya walimu 18 kuhojiwa na polisi, huku majalada ya watuhumiwa wanne yakitarajiwa kupelekwa kwa mwanasheria wa serikali kwa hatua zaidi. Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa walimu hao wanne, ni walimu wanafunzi kutoka vyuo tofauti vya ualimu. Lakini imefahamika pia kuwa kuna wengine wanaofuatiwa ambao wako Dar es salaam, hata hivyo kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya Bw Dhahiri Kidavashari amesema uamuzi kuhusu hatua zaidi, utachukuliwa na mwanasheria mkuu wa serikali.
Mradi wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 6 za Kenya – Daily nation- Kenya
Viongozi wa vyama vya upinzani na wale wa muungano tawala wa Jubilee nchini Kenya wameingia kwenye malumbano makali kuhusu mradi wenye thamani ya shilingi bilioni 6 za Kenya, unaojengwa mjini Murang’a ukiwa na lengo la kuongeza upatikanaji wa maji mjini Nairobi. Kiongozi wa muungano wa Cord Bw Raila Odinga amesema serikali inatekeleza mradi wa siri, ambalo utafanya miji mitano inayotumia mto Tana kubadilika kuwa jangwa. Waziri wa Maji Bw Eugene Wamalwa amemjibu Bw Odinga kwa kusema mradi huo ulizonduliwa mwaka 2012 na Bw Odinga mwenyewe alipokuwa waziri mkuu.
Mwanamke aliyuza pombe iliyosababisha vifo ahukumiwa kifo- The Standard – Kenya
Mwanamke aliyeuza pombe iliyosababisha vifo vya watu nane. Jaji Jessie Lessit amemkuta na hatia Bi Jennifer wanjiru Wang’anga ambaye miaka mitano iliyopita alitengeneza pombe iliyosababisha vifo vya watu nane. Bibi huyu anadaiwa kutengeneza pombe kwa kutumia viungo vyenye madhara kwa afya ya binadamu. Watu hao walikumbwa na maumivu makali baada ya kutumia pombe hiyo na kukimbizwa hospitali ambako walikutwa na mauti. Mtuhumiwa amekana makosa yake.
Post a Comment