Kuna mambo ukiyatafakari sana juu ya vilabu vyetu vikongwe nchini kati ya Simba SC na Yanga SC unaweza kubaki kinywa wazi hususani katika ile mizani ya upinzani wao wa jadi.

Akili ya haraka inaweza kukufanya utambue hawa ni maadui wakubwa katika uga wa soka nchini lakini ukifanya uchunguzi wa kisayansi unaweza kupata jibu tofauti na kubaki ukashangaa.

Mwanzoni mwa miaka ya 1925 kuendelea timu hizi hazikuwa na upinzani mkali uliopo sasa . Ingawa zote kipindi hicho hazikuwa na majina ya sasa , lakini chimbuko lao ndio linaanzia huko Yanga wakiitwa ' The Navigators baadae ' New Young ' Simba wakienda kwa jina la ' The Eagles '.

Yanga ikiwa timu ya mabaharia wa kiswahili na Simba ikijulikana kama timu ya Uhindini. Timu ya wadosi. Kulikuwa na upinzani kidogo sana kwa dhana moja tu ya wote kutawaliwa na sehemu kubwa na waafrika wakiungana kuleta upinzani kwa timu za kikoloni kama Arab FC na timu nyingine za serikali ya kikoloni.

Umaarufu wao , nguvu , ushawishi na kuleta upinzani kwa timu hizo na chagizo kubwa likiwa kutumika kisiasa na vyama vya ukombozi kama TANU kuliwafanya watawala wa kikoloni kuleta mfumo mpya wa kuzivunja nguvu Simba na Yanga ili kuondoa ukakasi huo.

Miaka ya 1932 mpaka 1936 ndipo mabadiliko makubwa kiutawala , mifumo ya uendeshaji , sera na kuzaliwa upya kwa vilabu hivi kulipoonekana au kutokea.

The New Young ( Young Africans SC ) jumatatu ya tarehe 11 Februari ilizaliwa upya na kuitwa Dar es salaam Young Africans Sports Club. Ikiwa klabu ya kwanza ya wazalendo kuendeshwa katika mfumo wa kisasa wa uendeshaji soka.

Mabadiliko haya yalitokana na maagizo ya kiintelejensia ya serikali ya kikoloni wakati huo ya sera yao ya ' divide and rule ' yaani wagawanye ili uwatawale vizuri. Sera hii ililenga kuvunja umoja wa vilabu vya kiafrika na kupandikiza chuki moyoni mwao.

Mwaka mmoja baadae yaani 1936 The Eagles now wakazaliwa upya kama Sunderland na kujenga misingi mipya ya kuzaliwa kwa klabu ya Simba SC ya sasa . Huu ndio mwaka rasmi uliozaliwa upinzani mkali wa jadi kati ya Yanga na Simba .

Yanga waliwaona wenzao kama wasaliti kwakuwa karibu sana na wadosi ambao enzi hizo walihesabika kama mabepari wa kikoloni . Kumbuka mwanzoni kabisa vilabu hivi vilikuwa na ushirika wa kupambana na vilabu vya kikoloni na serikali. Pia kupitia ushirika huo sera za kisiasa za ukombozi zilipenyezwa kwa kuwaunganisha vijana kwa wazee kutambua haki ya kudai Uhuru wao.

Bahati mbaya kwa kipindi kirefu baada tu ya kuzaliwa upya vilabu hivi , dunia iliingia katika mtikisiko wa vita kuu ya pili ya dunia 1939 mpaka mwaka 1945. Mambo mengi yalisimama yakiwemo ya soka .

Baada ya vita, 1946-48 ilianzishwa ligi daraja la kwanza mkoa wa Pwani na vilabu hivi kushiriki kikamilfu na wakati huu Simba walifanya tena mabadiliko ya jina lao na kuitwa Sunderland wakipata ufadhili toka kwa wadosi wa ng'ambo na hapo ndipo walipozidisha chuki na upinzani wao kwa Yanga . Ikiwa klabu ya kwanza nchini kuvaa viatu na jezi za kisasa.

Yanga waliendelea kubebana na wazawa wakipata sura ya utaifa licha ya ukata wao. Na hiki ndicho kiliwafanya viongozi wengi wa kisiasa kwenye harakati zao za ukombozi kuwa nao karibu.

Baada ya Uhuru viongozi wa kiserikali walitambua upinzani wa vilabu hivi unaweza kugeuka upinzani mbaya wa kisiasa na ndipo walipoanza kuvisogelea na kuviondolea makovu ya ukoloni na kuwarudisha katika njia moja ya upinzani kisoka.

Hatua mbalimbali zilichukuliwa ikiwemo kwa viongozi wakubwa wa kisiasa kutojihusisha moja kwa moja na soka kwa kukaa upande mmoja au kusaidia upande mmoja .

Baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 na mwaka uliofuata kuanzishwa kwa ligi daraja la kwanza yenye sura ya Jamhuri ya muungano kwa kushirikisha timu za bara na visiwani, Raisi wa Zanzibar wakati huo hayati Abeid Karume alianza kuwa karibu na vilabu vyote viwili yaani Yanga na Sunderland.

Ushawishi wake uliwafanya Sunderland kubadili jina lao na kuitwa Simba SC kuondoa ukiritimba wa kikoloni wa kutumia jina la klabu ya Sunderland ya England. Hii ilikuwa mwaka 1972. Mbali na kuwashawishi kubadili jina pia aliwapa ufadhili wa fedha za ujenzi wa jengo lao la makao makuu ya klabu hiyo akifanya hivyo pia kwa Young Africans SC chini ya kampuni ya Mecco.

Juhudi hizo ndio zilitumika kuviondoa vilabu hivyo katika mtazamo wa kisiasa enzi hizo za mfumo wa chama kimoja.

Kasumba hii ya kila linalofanyika Yanga lazima lifanyike na kwa wenzao ( Simba ) au Simba kwenda Yanga limeota mizizi mpaka leo.

Ukimuondoa mzee Karume aliyevifadhili vilabu vyote viwili, pia makampuni makubwa kama vile TBL nao pia wanaingia katika rekodi hiyo ya kuleta uwiano huo na kwa kizazi cha sasa kinashuhudia kampuni ya SportPesa ikifanya hivyo.

Kwa nyakati tofauti tumeshuhudia matajiri wa kihindi wakiongeza kasi katika upinzani wa vilabu hivi viwili.

Mwanzoni mwa miaka ya 90, hayati Abbasi Gulamali alimwaga fedha zake Yanga huku Simba wakitembea kifua mbele na mzee Azim Dewji.

Karne 21 bado mabosi wa kihindi wameendeleza upinzani huu wa jadi kwa namna yake . Yusufu Manji kwa Yanga na MO Dewji kwa Simba SC .

Haya yote yametokana na misingi ya upinzani huu iliyoweka mwaka 1936.

Post a Comment

 
Top