NYOTA wa muziki wa dansi na kiongozi wa bendi ya Malaika, Christian Bella, ameingia katika kashfa nzito ya kuwatelekeza baadhi ya wanamuziki wake katika ziara ya kimataifa iliyofanyika nchini Congo na Burundi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanamuziki hao walisema, baada ya baadhi ya shoo zao kukosa watu kutokana na mipangilio mibovu ya waandaaji, walilazimika kuishi maisha magumu ya kulala na njaa, huku wengine wakishikiliwa na wamiliki wa hoteli kutokana na kudaiwa fedha za malazi.
Walisema wakiwa Congo, Bella alisusia kupanda jukwaani kwa kile alichodai kuona mashabiki waliojitokeza ni wachache, hatua iliyomfanya kutumia hali hiyo kama kisingizio cha kuwanyima posho na kuwatelekeza ughaibuni.
“Alichotufanyia Bella Mungu anamuona, kwani tukiwa Congo alitukimbia na kurudi Dar es Salaam akituacha kwenye wakati mgumu, huku baadhi yetu wakiwekwa rehani ili kushinikiza kulipwa fedha za malazi katika hoteli tuliyopangiwa na Kiongozi wetu,” alisema.
Alisema baada ya Bella kurudi Dar es Salaam alikata mawasiliano nao, kabla ya kuwatumia pesa kidogo ambayo walijibana na kufanya nauli ya kurudi huku, ambapo wenzao wawili wanaendelea kushikiliwa mpaka sasa kutokana na deni la hoteli.
Tulimtafuta Christian Bella, ambaye alidai hawafahamu wanamuziki hao na hajaingia mkataba na msanii yeyote kutoka ndani ya bendi hiyo.
“Siwezi kucomment yes au no, lakini ukweli siwafahamu na sijawahi kuingia mkataba na msanii yeyote, ingawa hii bendi ya Malaika namiliki mimi,” alisema.
Alipotafutwa mmoja wa viongozi wa bendi hiyo, Andrew Sekedia, ambaye naye alikumbwa na mkasa huo, alipatwa na kigugumizi na kusema hayuko tayari kuzungumzia jambo hilo.
Post a Comment