Juma lililopita gwiji la Azam FC John Rafael Bocco al maarufu kama ‘ Adebayor ‘ aliandika kwenye akaunti yake ya istagram ujumbe wa kuonesha kuichoka timu yake na maneno mengine yaliyoashiria kuondoka katika timu hiyo tena katika hali ya ugomvi. Licha ya klabu yake ya Azam FC kutengua kauli yake na kusema nahodha wao huyo akaunti yake ilikuwa imeingiliwa na wahuni lakini mwisho wa siku John Bocco alisepa.

Kama iliyokuwa kwa nahodha huyo , usiku wa leo kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Salumu Aboubacary maarufu kwa jina la ‘ sure boy ‘ akirithi jina la utani la baba yake aliyevuma vilivyo na klabu ya Yanga , nae pia ameandika maneno yale yale kwenye akaunti yake ya Istagram. Sehemu ya maneno hayo inasema ;

” ….mtu hawezi kujua thamani ya kitu mpaka akikose. Ukiona mwenzio kanyolewa zako tia maji….”

Ukitafakari maneno haya kwa kina na ukioanisha na maneno ambayo aliandika John Bocco ni dhahiri kiungo huyo anaifuata njia aliyopita John Bocco kuondoka hapo Chamazi.

Kama ilivyokuwa kwa wakongwe wengine ndani ya kikosi hicho cha Azam FC mabingwa wa kombe la Kagame 2015-16 mikataba yao inakwenda ukingoni mwezi ujao na hakuna dalili ya kuongeza kutokana na mfumo wa usajili kuwakwaza wachezaji wengi na mawakala wao, ndicho kinachomsumbua pia Salumu Aboubacary.

Tayari kipa namba moja wa timu hiyo Aishi Manula anahusishwa kujiunga na wekundu wa Msimbazi Simba SC kwa dau nono la milioni 100! kama ilivyokuwa kwa John Bocco ambaye inasemekana amekwisha malizana na washindi hao wa kombe la Shirikisho mwaka huu na wanasubiri tu kipindi cha usajili kianze waweke mambo hadharani.

Uongozi wa Azam FC juma lililopita walitoa taarifa ya kupandisha vijana watano kutoka timu B kuja timu kubwa kwa ajili ya msimu mpya wa ligi utakaoanza mwezi wa nane mwaka huu hiyo yote ni katika kujiweka sawa na kukimbiwa na nyota wake ambao wanaonekana kuugomea mfumo mpya wa usajili klabuni hao ambao unawataka kuchukua nusu ya mishahara yao mwanzoni tu mwa kuongeza mkataba mpya na malipo mengine yatategemea uwezo wako uwanjani.

Sure boy amedumu katika kikosi cha Azam FC kwa miaka mingi akisimama vyema kama kiungo mchezeshaji na mshambuliaji wa timu hiyo . Msimu wa 2013-14 Azam FC wakiibuka mabingwa wa ligi kuu nchini chini ya Joseph Omog , ndio alikuwa injini ya timu akiwachezesha vyema John Bocco na Kipre Tcheche. Endapo Azam FC watamwachia kijana huyo kutimka kikosi hapo ni dhahiri Simba SC , Yanga SC na Singida United wanaweza inyatia kandarasi ya mchezaji huyo.

Post a Comment

 
Top