UKISIKIA jeuri ya fedha ndiyo hii. Yanga waliwekewa mezani fedha za udhamini kiasi cha Sh milioni 800kwa mwaka, sawa na Sh bilioni 4 kwa miaka mitano na kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportsPesa, wakachomoa na kudai waongezwe zaidi ili kuendana na hadhi ya klabu hiyo.
SportsPesa, ambao ni wadhamini wa klabu ya Gor Mahia na FC Leopards za Kenya pamoja na klabu ya Ligi Kuu nchini Uingereza, Hull City, imeanza shughuli zake hapa nchini tangu wiki iliyopita.
Kampuni hiyo ya michezo ya kubahatisha iliyachukua mapendekezo ya Yanga na kuyapitia, kisha ikakubali kuingia kwenye dili na sasa huenda pande hizo mbili zikasaini mkataba rasmi leo Jumatano ambao utakuwa ni mkubwa zaidi ya ule wa watani wao wa jadi, Simba, waliokubali kusaini kwa dau la Sh milioni 880 kwa mwaka, ambazo ni sawa na Sh bilioni 4.9 kwa miaka mitano.
Habari za uhakika ambazo gazeti la DIMBA Jumatano limezipata zinaeleza kuwa, awali SportsPesa walianza kuwafuata Yanga na kuzungumza nao kwa ajili ya kutaka kuwadhamini, lakini viongozi wa klabu hiyo ya Jangwani wakachomoa baada ya kuona pesa ni ndogo na hivyo kutoa masharti mapya.
Kwa mujibu wa habari hizo, SportsPesa waliipa Yanga ofa ya Sh 800 milioni kwa ajili ya kuidhamini, lakini mabosi wa timu hiyo wakakataa na badala yake wakataka kupatiwa Sh bilioni 1.2 pamoja na mahitaji mengine nje ya hapo.
Katika mahitaji yake, Yanga ilitaka kupewa kiasi hicho cha fedha pamoja na basi lenye thamani ya Sh 350 milioni, jambo ambalo baadaye limeonekana kukubaliwa na wadhamini hao.
Kutokana na hali hiyo, sasa Yanga huenda kuanzia leo Jumatano ikaanza kudhaminiwa na kampuni hiyo kwa kitita cha Sh bilioni 1.2 kwa mwaka, ambazo ni sawa na Sh bilioni 6, dau ambalo ni kubwa kuliko lile walilopata mahasimu wao, Simba, ambao wamepata sh bilioni 4.9.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka kwa watu wa ndani wa Yanga na SportsPesa, dau la Sh bilioni 1.2 limewalainisha Yanga kuweka nembo ya SportsPesa katika jezi zao.
Hiyo inamaanisha kwamba, Yanga watavuna zaidi ya Sh bilioni 6 katika kipindi cha miaka mitano, huku wakivuna angalau kiasi cha Sh milioni 100 kwa mwezi.
Kitita cha Yanga ni sawa na ongezeko la asilimia 36 kulinganisha na kiasi walichopewa Simba, ambao watakuwa wakivuna Sh milioni 74.5 kwa mwezi.
Kwa hesabu hizo, Yanga watakuwa wakichota Sh milioni 25 zaidi ya Simba kila mwezi, hivyo kuwa na fungu kubwa zaidi la kuendesha mambo yao.
Inawezekana Yanga wamepata dau kubwa zaidi ya Simba kwa kuwa tayari jezi zao zilikuwa na mdhamini, Quality Group, tofauti na watani wao ambao jezi zao zilikuwa tupu kwa mwaka mzima tangu mkataba wa Kilimanjaro Lager ulivyomalizika.
Kutokana na udhamini huo, Yanga inakuwa klabu ya kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati kudhaminiwa kwa dau kubwa kuliko klabu yoyote. Kwa mujibu wa rekodi zilizopo, udhamini mkubwa wa SportsPesa uko kwa klabu ya Gor Mahia ya Kenya, ambayo inapewa kitita cha Sh za Kitanzania bilioni 1.1 kwa mwaka na kufuatiwa na AFC Leopards (900 milioni), huku Simba ikipata Sh milioni 880 kwa mwaka.
Ili kupata ukweli kuhusiana na dili hilo, Jumamosi iliyopita gazeti la DIMBA Jumatano lilizungumza na mmoja wa Wakurugenzi wa SportsPesa, Tarimba Abbas, ambaye hata hivyo hakupenda kuweka wazi suala hilo kwa madai kuwa bado wakati wake.
“Sisi kama SportsPesa, tunahitaji kuleta changamoto mpya katika soka la Tanzania, kwa hiyo kusema tutaidhamini klabu gani nyingine baada ya Simba, bado wakati wake, lakini lengo letu ni kudhamini klabu moja au nyingi, ila wakati ukifika mtaona tunatangaza,” alisema Tarimba.
Naye Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, alipoulizwa jana kuhusiana na dili hilo, alikataa kusema chochote zaidi ya kusisitiza kwamba, kuna kitu cha surprise ‘kushtukiza’ kitafanyika leo saa sita mchana kwenye makao makuu ya klabu, ingawa hakusema ni nini.
Awali, Yanga ilikuwa na udhamini wa kampuni ya TBL ambao ulikoma msimu uliopita, ambapo ilikuwa ikipata Sh 500 milioni kwa mwaka, fedha ambazo zilikuwa zikitoka kwa mgawanyo wa kila mwezi.
Baada ya udhamini huo kukoma, Yanga ilipata udhamini wa muda mfupi kutoka kwa kampuni za Quality Groups, zinazomilikiwa na Mwenyekiti wake, lakini mapema Februari ilitangaza tenda ya kutaka kupata udhamini mpya.
Post a Comment