UONGOZI wa Majimaji ya mjini Songea umeitolea nje Azam FC baada ya kuwaambia kuwa hawako tayari kumwachia kocha wao mkuu, Kalimangonga ‘Kally’ Ongala.
Wiki iliyopita Azam ililifuta kazi benchi zima la ufundi kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika Ligi Kuu Bara, ambapo inakamata nafasi ya sita.
Makocha waliotimuliwa ambao ni raia wa Hispania ni Zeben Hernandez wengine ni Yeray Romero, kocha wa makipa Jose Garcia, kocha wa viungo, Pablo Borges na mtaalamu wa tiba za viungo, Sergio Perez.
Mwenyekiti wa Majimaji, Humphrey Milanzi, ameliambia BINGWA kuwa Azam iliwasilisha kwao nia ya kumhitaji Ongala ili aweze kuziba nafasi ya Hernandez, lakini wamekataa kumwachia kwa wakati huu kwa vile bado wanamhitaji.
“Tumewaeleza kama wanamhitaji Ongala wasubiri hadi ligi ifike ukingoni ndipo waje, tutazungumza nao kwa kuwa mkataba wake utakuwa umebaki nusu msimu lakini kwa sasa hapana.
“Ikumbukwe mzunguko wa kwanza Majimaji haikufanya vizuri ndio maana tuliamua kumrejesha Ongala ambaye alitusaidia kuibakisha timu msimu uliopita, pia Ongala amefanya kazi na sisi miezi miwili tu tangu arudi tunawezaje kumruhusu aondoke wakati malengo ya kumleta tena hayajatimia,“ alisema bosi huyo.
Sorce-bingwa
Post a Comment