Rais Maghufuli aendelea kudhihirisha kwa vitendo ahadi zake- Habari Leo - Tanzania
Serikali ya Rais John Magufuli imefanya jambo ambalo halijafanyika kwa muda mrefu, yaani kuanza kulipa deni la nje, chini ya mwaka mmoja akiwa madarakani. Hii ilikuwa ni moja ya ahadi iliyotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi. Takwimu zilizotolewa na ofisi ya takwimu ya taifa NBS na gavana wa benki kuu ya Tanzania Prof Benno Ndulu zinaonyesha kuwa uchumi umeimarika kiasi kwamba serikali imekuwa na uwezo wa kuanza kulipa deni ambalo limepigiwa kelele sana na wapinzani. Gavana Ndulu amesema BoT imeanza kulipa madeni yote ya ndani na nje kwa fedha zake za ndani ambapo tayari imeshalipa kiasi cha Sh bilioni 96 za deni la ndani, na dola za Kimarekani milioni 90 za deni la nje.

Waziri Mkuu wa Tanzania aagiza nyumba za tope ziondolewe katikati ya mji wa Dodoma - Nipashe - Tanzania.
Waziri Mkuu wa Tanzania Bw Kassim Majaliwa ameagiza nyumba za udongo zilizopo katikati ya mji wa Dodoma ziondolewe, na watakaopewa viwanja vya nyumba hizo kama hawataendeleza watanyanganywa. Waziri mkuu ameiagiza mamlaka ya uendelezaji wa makao makuu CDA kuweka utaratibu wa kuwapatia ardhi wanaohitaji, na kuwakumbusha wakazi wa Dodoma kutumia fursa ya sasa kujipatia mitaji. Waziri Majaliwa amesisitiza kuwa serikali imehamia Dodoma na mtu yoyote atakayetaka huduma ya kutoka ofisi ya waziri mkuu bila kujali yeye ni nani, anatakiwa kwenda Dodoma.

Makamishna wa tume ya ukweli na maridhiano wana wasiwasi ripoti ya tume inaweza kuleta matatizo- Daily Nation – Kenya
Ripoti ya tume ya maridhiano na ukweli imesema ina wasiwasi kuwa ripoti yake inaweza kuleta matatizo kwenye siasa za Kenya, kwani yaliyomo yanawagusa wanasiasa waliopo kwenye muungano tawala wa Jubilee na wale wa upinzani wa Cord. Ripoti hiyo ambayo haijawahi kuwasilishwa kwenye bunge la Kenya inatoa mwito wa kuchukuliwa kwa hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kufungua kesi za zamani. Makamishana hao wamesema hayo baada ya kiongozi wa Muungano wa Cord Bw Raila Odinga kutoa mwito wa kufikisha ripoti hiyo mbele ya bunge na kupitishwa.

Mgogoro wa ardhi Mombasa waleta migongano kati ya maofisa wa serikali- Standard.
Mgogoro wa ardhi kati serikali ya Kaunti ya Mombasa, Shirika la utangaza la Kenya KBC na mtu wa tatu, umeingia katika sura mpya baada ya mratibu wa kaunti ya Mombasa Bw Nelson Marwa kutishia kumtia mbaroni gavana wa Mombasa Bw Hassan John ambaye aliamuru ukuta uliojengwa na KBC ubomolewe. Bw Marwa amesema Gavana John anatumia suala hilo kwa manufaa yake kisiasa na hamfanyi juhudi zozote kutatua mgogoro huo. Bw Marwa amesema serikali ya Kaunti ilikodi wahuni kwenda kubomoa.

Wabunge wawaita wahariri kutoka maelezo ni kwanini wanaandika habari zisizo na uwiano kuhusu bunge- Obsever- Uganda
Bunge la Uganda limewaita wahariri wa vyombo vinne vya habari vya Uganda kutoka maelezo kwa kile walichokiita habari hasi na zisizo na uwiano kuhusu bunge. Mbali na gazeti hili la Obsever, vyombo vingine ni gazeti la Daily Monitor, Red Pepper na Uganda Radio Network. Hatua hiyo imefikia baada ya malalamiko kutoka kwa spika wa bunge Bibi Rebecca Kadaga na wabunge wengine kuhusu ripoti inayohusiana na matumizi ya fedha za wabunge kwenye mkutano uliofanyika Boston Marekani. Wote wanatakiwa kufika tarehe 5 Oktoba mbele ya kamati ya kanuni, stahili na wajibu ya bunge la Uganda.

Wabunge Uganda wasema hospitali ya rufaa ya Mbarara ina hali mbaya- Daily Monitor- Uganda
Wajumbe wa kamati ya mahesabu ya bunge la Uganda wamegundua madudu baada ta kufanya ziara ya ghafla katika hospitali ya rufaa ya Mbarara. Wabunge hao waliofanya ziara ya ghafla walikuta kuna nesi mmoja tu wa zamu, na wengine walikuwa wakichelewa kazini, na kutaka hatua za haraka zichukuliwe kuondoa hali hiyo. Wabunge hao ambao pia waliongea na wagonjwa walipokea malalamiko kutoka kwa wagonjwa wanaotozwa fedha kwa ajili ya vitanda na dawa, licha ya serikali kupiga marufuku utaratibu huo.

Kanuni mpya za asili ya bidhaa kuchochea maendeleo ya viwanda katika nchi za Afrika Mashariki- NewTimes-Rwanda
Kanuni zilizopitiwa upya kuhusu asili ya bidhaa zinazozalishwa katika nchi za Afrika Mashariki zimehimiza sekta ya uzalishaji viwandani. Wakiongea kwenye mkutano wa 7 wafanyabiashara wa Afrika Mashariki uliofanyika mjini Kigali, wafanyabiashara wa jumuiya hiyo wamesema kanuni ya 25 kuhusu biashara iliyoanza kutekelezwa mwezi januari mwaka jana, imekuwa na mchango katika kuhimiza maendeleo ya viwanda. Ofisa mkuu wa idara ya forodha ya Rwanda Bw Fred Nuwagaba amesema kanuni za sasa zina unyumbufu, ziko wazi na zinajieleza. Hata hivyo waziri wa mambo ya Afrika Mashariki Bibi Valentine Rugwabiza amesema bidhaa zinazoalishwa kwenye eneo la Afrika Mashariki zinatakiwa kuongezewa thamani ili ziweze kunufaika zaidi na nafuu ya kodi.

Mahakama ya Afrika Mashariki haitatoa hukumu kuhusu awamu ya tatu ya Rais Nkurunziza –IWATSU- Burundi
Mahakama ya Afrika Mashariki imesema haitatoa hukumu kuhusu malalamiko yaliyowasilishwa kuhusiana na kipindi cha tatu cha Rais Pierre Nkurunziza, na kusema kwa sasa hayana msingi. Mahakama hiyo imesema haiwezi kutoa hukumu kuhusu kesi hiyo kwa kuwa tayari mahakama za Burundi zimetoa uamuzi. Mahakama hiyo imesema malalamiko hayo yametolewa baada ya muda kupita na sasa haiwezi kutolea uamuzi jambo lililoamuliwa.

Post a Comment

 
Top