Uongozi wa klabu ya Simba umeshindwa kutoa ufafanuzi kuhusu suala la kocha wao msaidizi Jackson Mayanja aliyeachia ngazi hii leo kutokana na sababu zilizosemekana kuwa ni za kifamilia.
Baada ya taarifa hizo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kung'atuka kwa Mganda huyo mtandao huu ulifanya jitihada za kuwatafuta viongozi wa Wekundu hao (katibu, meneja na msemaji) kutoa ufafanuzi lakini simu zao ziliita bila kupokelewa.
Mchezaji mmoja wa Simba ambaye hakutaka jina lake kuandikwa kwenye mtandao huu alisema kocha huyo aliwaaga jana usiku akisema anajiweka pembeni kutokana na matatizo ya kifamilia.
"Ni kweli kocha Mayanja ametuaga jana amesema anajiweka pembeni kutokana na matatizo ya kifamilia nasi tumemtakia kila la kheri," alisema nyota huyo.
Mtandao huu pia ulimtafuta Mayanja mwenyewe kuthibitisha taarifa hizi lakini nae alishindwa kupokea simu yake.
Jitihada za kuwatafuta viongozi wa Simba kulitolea ufafanuzi suala hili bado zinaendelea.
Source: simba damu
Post a Comment