SIMBA wameiangalia kwa umakini safu yao ya ushambuliaji baada ya kumsajili John Bocco, a aka gun day kuwa, yeye peke yake atakuwa na mzigo mkubwa wa kupachika mabao na sasa wagmeingia msituni kumtafutia pacha ywake.
Wekundu hao wa Msimbazi wamemsajili Bocco kutoka Azam FC, ambapo atashirikiana na Laudit Mavugo kwenye safu ya ushambuliaji na sasa uongozi unatafuta mtu mwingine wa maana wakati huu wa usajili.
Na katika majina ambayo Simba wameyakazia macho, lipo la straika Mtanzania anayekipiga nchini Kenya katika Klabu ya Sonny Sugar, Abdallah Khamis, ambaye anao uwezo mkubwa wa kucheka na nyavu.
Kigogo mmoja wa Simba ameliambia DIMBA Jumatano kwamba, kama kuna watu walidhani baada ya kuondoka Ibrahim Ajib na kujiunga na Yanga watakuwa wamekwama, itakula kwao, kwani sasa hivi wapo mawindoni kusaka injini nyingine ya maana.
“Ni kweli katika safu yetu ya ushambuliaji tunataka kuongeza mtu mwingine atakayesaidiana na Bocco, yapo majina mengi ambayo tunayo, likiwamo hilo la Abdallah Khamis, nadhani ndani ya siku chache hizi tunaweza kukamilisha usajili huo.
“Msimu huu tumedhamiria kufanya mambo makubwa, ndiyo maana usajili wetu umezingatia uwezo, nidhamu pamoja na kujituma, hakuna shaka mashabiki wetu watafurahi wenyewe msimu ujao,” alisema.
Akizungumzia ujio wa Mganda Emmanuel Okwi, kigogo huyo alisema mambo yanakwenda vizuri na kama kuna watu wanadhani uongozi umejaa wababaishaji wataumbuka wenyewe, kwani wanafanya mambo yao kisomi zaidi.
“Kuna watu wanadhani tunadanganya, lakini niwaambie tu, sisi tupo makini sana, ndiyo maana tukafanikisha usajili wa watu kama Bocco, Kapombe (Shomari), Aishi Manula na wengineo, Okwi mtamuona akiichezea Simba msimu ujao,” alisema.
Simba, ambao wamefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya FA, wataiwakilisha nchi Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani, ndiyo maana wanakomaa kufanya usajili wa nguvu ili kufika mbali na kuepuka kuishia hatua za awali.
Post a Comment