SIMBA wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanamalizana na straika Mzimbabwe, Donald Ngoma, kwani walishafanya naye mazungumzo ya awali, huku Yanga nao wakifanya kila linalowezekana kumbakisha straika wao huyo, ambapo taarifa zilizopo zinadai kuwa Mzimbabwe huyo yupo mafichoni nchini Afrika Kusini.

Ngoma amemaliza mkataba wake na Yanga, ndiyo maana Simba wameingia kwa nguvu zote wakitaka huduma yake kwa ajili ya msimu ujao, huku pia wakijua kwamba wanakabiliwa na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Taarifa za uhakika kutoka Simba zinadai kuwa, mazungumzo ya awali kati yao na mchezaji huyo yameshafanyika na haitashangaza msimu ujao akiwa amevalia uzi mwekundu na kuukacha ule wa njano unaotumiwa na Yanga, huku pia Haruna Niyonzima naye akijumuishwa kwenye rada hizo.

Tunafahamu kwamba, idadi kubwa ya wachezaji wa Yanga, hasa wale wenye majina makubwa, mikataba yao imefikia tamati, ndiyo maana baadhi ya timu zimekuwa zikihaha kutafuta saini zao.

Wakati Simba wakiweka mpango mkakati huo wa kumnasa Ngoma pamoja na Niyonzima, Yanga nao wamekuwa na vikao vya mara kwa mara kati ya kamati ya utendaji na ile ya usajili, lengo likiwa ni kuwazuia wachezaji wao muhimu wasiende popote.

Hata hivyo, taarifa zisizo na shaka zinadai kuwa, kwa sasa Ngoma yupo nchini Afrika Kusini na haijulikani kwamba yupo huko kwa lile dili lake la siku nyingi la kutakiwa na Mamelod Sundown, au kuna timu nyingine imemficha huko.

Kigogo mmoja wa Yanga amesema kwamba, straika wao huyo yupo nchini humo, lakini amewafungia vioo, kwani hataki kuwasiliana nao, kitu ambacho kinaashiria kuwa anaweza akawapa mkono wa kwaheri.

“Taarifa zake zipo na tuna uhakika kwamba yupo nchini Afrika Kusini na yupo huko kwa ajili ya mambo yake binafsi, lakini huwa mara kwa mara hataki kuwasiliana na sisi, amekuwa mgumu sana sijui kwanini,” alisema kwa ufupi kigogo huyo.

Kuhusu Niyonzima, kigogo huyo alisema Mnyarwanda huyo amekuwa akiwasiliana na kila mtu ndani ya Yanga kwa njia ya simu, kwani asipopigiwa, yeye anaweza akapiga, kitu ambacho kinaonyesha kwamba yupo tayari kuendelea kuitumikia timu hiyo.

“Kwa Haruna (Niyonzima) kusema ukweli amekuwa muungwana sana, kwani licha ya kwamba mkataba wake umemalizika, lakini tumekuwa tukiwasiliana kila mara, tusipopiga simu sisi, basi yeye atapiga, tunazungumza mengi, kwani hapa Tanzania ni kama nyumbani kwao.

“Kwa ujumla uongozi unafanya kila linalowezekana kuhakikisha wale waliomaliza mikataba yao wanaongezewa mingine, Haruna Niyonzima ni mmoja wa wale ambao nadhani tutaendelea kuwatumia msimu ujao,” alisema.

Ngoma na Niyonzima ni kati ya wachezaji walioiletea heshima kubwa Yanga kutokana na uwezo wao ndani ya Uwanja, lakini huenda Wanajangwani hao wakapata pigo kama hawatafanya jitihada za nguvu kuwaongezea mkataba.

Hata hivyo, huenda wakapata unafuu wa kumuongezea mkataba Niyonzima kuliko Ngoma, ambaye alishaweka wazi kwamba atatimka na moja ya timu iliyoonyesha nia ya kumnasa ni Mamelod ya nchini Afrika Kusini, ambapo Straika huyo yuko huko, huku pia Simba nao wakiingiza mkono wao kuitaka saini yake.

Post a Comment

 
Top