UONGOZI wa Simba umemleta nchini beki wa kati kutoka Rwanda, Munezero Fiston, kurithi nafasi ya Method Mwanjali, ambaye yuko mbioni kutemwa na sasa jukumu la kumchambua kama anafaa ama la ameachiwa kocha Mkuu wa kikosi hicho, Joseph Omog.

Fiston alitua nchini Jumapili ya wiki iliyopita na Jumatatu asubuhi alikwenda katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika Uwanja wa Chuo cha Polisi, kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya SportPesa Super Cup.

Kigogo mmoja ndani ya  Simba kwamba, bado hawajampa mkataba beki huyo mpaka pale Omog atakapojiridhisha kuwa Mnyarwanda huyo atamfaa mbele ya safari.

“Tunachoweza kusema ni kwamba, sisi kama uongozi hatuwezi kumuamulia kocha na badala yake kile anachokitaka ndicho tunakifanya, yeye alipendekeza tusajili beki mmoja, nasi tumemleta huyo na kilichobaki ni yeye ampime kama atamfaa,” alisema.

Taarifa zilizopo zinadai kuwa, huenda Simba wakamtema Method Mwanjali, kutokana na majeraha ya muda mrefu yanayomkabili, huku pia Jjuuko Murushid naye akitajwa kutaka kuikacha timu hiyo.

Katika safu hiyo ya beki wa kati, Simba wapo Mwanjali, Jjuuko pamoja na Abdi Banda, ambao wote hawana uhakika wa kuendelea kuitumikia timu hiyo, huku mashabiki wakikosa kabisa imani na Novaty Lufunga, kutokana na makosa yake ya mara kwa mara yanayoigharimu timu.

Wekundu hao wa Msimbazi wanataka kujiimarisha zaidi kutokana na kukabiliwa na michuano ya Kimataifa ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika mwakani, lakini pia wakitaka kufanya vizuri Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Mara ya mwisho kwa Simba kushiriki michuano ya kimataifa, ilikuwa mwaka 2013, ambapo tangu hapo wamekuwa watazamaji tu, wakiwaangalia Yanga na Azam FC, lakini sasa bahati imewaangukia na mwakani wataiwakilisha nchi Kombe la Shirikisho Afrika.

Post a Comment

 
Top