RAIS wa Simba, Evance Aveva, ambaye hana kawaida ya kuzungumzia masuala mbalimbali ya klabu hiyo, juzi alifunguka na kudai kwamba kasi yao ya usajili ipo palepale na wanaosema labda wamepunguzwa spidi basi itakula kwao.
Simba ilianza kutangaza usajili wa mwendo kasi kwa kuivamia klabu ya Azam FC na kusajili wachezaji watatu tegemeo, straika John Rafael Bocco, kipa Aishi Manula na beki kisiki Shomari Kapombe.
Siku mbili tatu zilizopita, kibao kikawageukia wao, ambapo mahasimu wao, Yanga, nao wakapeleka kilio Msimbazi kwa kumsajili mchezaji kipenzi cha mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi, Ibrahim Ajib na hapo maneno yakaanza kwamba Simba imenyamazishwa.
Akizungumza juzi katika hafla maalumu ya klabu hiyo kwa wanachama, wachezaji pamoja na wadau wa klabu hiyo iliyofanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Dar, Aveva alisema kazi bado mbichi, kwani nia yao ni kuhakikisha wanasajili Simba itakayokuwa ya kimataifa.
Licha ya kusajili nyota hao kutoka Azam, klabu hiyo pia imeshamalizana na Jamal Mwambeleko, Yusuf Mlipili pamoja na Ally Shomari kutoka Mtibwa Sugar, huku taarifa za uhakika za kumrejesha straika wake wa zamani, Emmanuel Okwi, zikizidi kukamilika.
Tayari Okwi ameshafanya mazungumzo ya kina na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope, aliyesafiri hadi jijini Kampala, nchini Uganda kwa ajili ya kumaliza zoezi hilo.
Katika hatua nyingine, Aveva aliwataka Wanasimba watulie katika kipindi hiki ambacho viongozi wamejipanga kurudisha heshima ya klabu yao, ambapo pamoja na kazi kubwa ya usajili, lakini pia nguvu za ziada zinatarajiwa kuelekezwa katika ujenzi wa uwanja wa kisasa wa klabu hiyo, uliopo Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
“Muda wowote kuanzia sasa tutaleta ajenda hii mezani ya kuhakikisha tunatandika nyasi zetu katika Uwanja wa Bunju kwa ushirikiano mzuri na umoja wetu kama ilivyokuwa katika suala la kusapoti timu, kikubwa hapa ni kudumisha ushirikiano,” alisema.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dionis Malinzi, amewataka viongozi wa Simba kuwa makini katika suala la usajili, ili waepuke kusajili wachezaji mamluki wasiokuwa na mapenzi na klabu hiyo.
Malinzi, ambaye pia ni mwanachama wa Simba, alisema: “Siku zote ukikosea kwenye usajili inaweza kukugharimu, ndiyo maana nawaasa kuwa waangalifu, msajili wachezaji wenye mapenzi mema na timu, la sivyo itakuwa ni hasara,” alisema.
Post a Comment