Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga , wameeleza nia yao ya kutumia asilimia kubwa ya wachezaji wa kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20 kwenye michuano ya kombe la SportPesa inayotarajiwa kuanza wiki ijayo.
Yanga wameeleza kua uamuzi huo unakuja baada ya baadhi ya wachezaji wao kujiunga na kikosi cha timu ya taifa huku wengine wakiwa wamemaliza mikataba yao huku kukiwa na uwezekano wa kusajiliwa na timu nyingine .
Yanga imepangwa kufungua na mabingwa wa Kenya, Tusker, Juni 5. Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alisema kuna wachezaji wengi wazuri wa timu yao ya vijana ambao watatumia fursa hiyo kuonesha vipaji vyao kwa kushirikiana na wachezaji wazoefu.
Mbali na Yanga, wanaoshiriki michuano hiyo timu nyingine za Tanzania ni Simba, Singida United na Jang’ombe Boys ya Zanzibar.
Aidha, timu za Kenya zitakazoshiriki ni Gor Mahia, AFC Leopards, Tusker na Nakuru All Stars. Yanga baada ya kutwaa ubingwa wa ligi walifanya ziara Dodoma na Arusha ambapo walirudi Dar es Salaam juzi na wakati wowote wataanza mazoezi ya kujiandaa na michuano hiyo. Bingwa wa michuano hiyo anatarajiwa kucheza na Everton inayocheza Ligi Kuu ya England
Post a Comment