HABARI njema kwa mashabiki wa Simba ni kwamba mfanyabiashara bilionea, Mohammed Dewji ‘Mo’, amerejea Simba ili kuisaidia timu hiyo kwa ajili ya mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mbao FC.
Kulikuwa na hofu kubwa baada ya tajiri huyo kutoa dukuduku lake kufuatia mkataba ambao Simba waliingia na kampuni moja ya ‘kubetisha’ bila ya yeye kushirikishwa, lakini sasa matumaini ya klabu hiyo ya Msimbazi kupanda ndege kwa ajili ya michuano ya kimataifa yamerejea.
Baada ya Dewji kurejea, mikakati ya kuibuka na ushindi kwenye mechi hiyo ya fainali itakayochezwa Mei 27, mwaka huu katika Uwanja wa Jamuhuri mkoani Dodoma, imeanza kwa klabu hiyo ili kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa.
Akithibitisha kumalizika kwa suala hilo, Makamu wa Rais Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, alisema kwa sasa klabu hiyo haina mgogoro tena na wapo kitu kimoja na tajiri wao huyo.
“Tulishamalizana na sasa wote tunaongea lugha moja, nadhani huu ni wakati sahihi wa kuungana ili kufanya vizuri kwenye mechi zetu mbili zilizobaki,” alisema.
Kaburu alisema kwa sasa nguvu zao wanazielekeza kwenye michezo yao miwili, ambao ni ule wa Ligi Kuu dhidi ya Mwadui utakaochezwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na ule wa Mbao FC.
“Michezo yote miwili iliyosalia ni muhimu, hivyo tunapaswa kushinda dhidi ya Mwadui ule wa fainali na kutupa nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika,” aliongeza Kaburu.
Post a Comment